SOKA ni mchezo wenye wapenzi wengi barani Afrika kama ilivyo kwa mabara mengine.
Afrika, tuna mashindano yetu ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN), yaani African Cup of Nations.
Mashindano haya, hukutanisha timu za taifa za nchi za Afrika, ambayo hufanyika kila baada ya miaka miwili.
Historia ya Kombe la Mataifa ya Afrika, ilikuwa chimbuko la kikao cha watu saba kilichofanyika Lisbon, Ureno mwaka 1956.
Tangu kuasisiwa na kufanyika kwa mara ya kwanza kwa fainali hizi mwaka 1957 nchini Sudan, ni fainali ambazo zimekuwa zikipata umaarufu kila zinapofanyika.
Kabla ya kuanza mashindano haya ambayo safari hii yalifanyika Ghana, kuanzia Januari 20 hadi Februari 10, yalitakiwa kuwakilishwa na nchi nne, ambazo ni Misri, Sudan, Ethiopia na Afrika Kusini, ambayo baada ya kugubikwa na sera ya ubaguzi wa rangi, iliondolewa.
Baada ya hapo mashindano hayo yameonyesha kufanikiwa zaidi, kwani idadi ya washiriki ilizidi kuongezeka mwaka hadi mwaka kuanzia nchi 3, 6, 12 na sasa 16.
Nchi zilizoandaa fainali hizi ni kama ifuatavyo, mwaka 1957 (Sudan), 1959 (Misri).
Mwaka 1962 (Ethiopia), na mwaka 1963 (Ghana), ambao pia ndio waliandaa fainali za mwaka huu, zilizokwisha kwa Misri kutetea ubingwa kwa kuifunga Cameroon 1-0.
Mwaka 1965, fainali hizo zilifanyika nchini Tunisia na 1968, zilipigwa kwa mara ya pili nchini Ethiopia.
Fainali za mwaka 1970, zilifanyika kwa mara ya pili Sudan na mwaka 1972, zilifanyika nchini Cameroon.
Mwaka 1974, Misri iliandaa tena fainali, na mwaka 1976, zilifanyika nchini Ethiopia.
Mwaka 1978, fainali zilifanyika nchini Ghana, na mwaka 1980, zilifanyika Nigeria.
Fainali za mwaka 1982, ziliandaliwa na Libya na fainali za mwaka 1984 zilifanyika nchini Ivory Coast.
Mwaka 1986, fainali zilifanyika Misri na mwaka 1988, zilifanyika Morocco kabla ya zile za mwaka 1990, zilizofanyika Algeria.
Mwaka 1992, fainali hizi zilifanyika Senegal kabla ya zile za mwaka 1994, zilizofanyika Tunisia.
Mwaka 1996, zilifanyika Afrika Kusini, kabla ya zile za mwaka 1998 zilizofanyika nchini Burkina Faso.
Za mwaka 2000, ziliandaliwa kwa pamoja na nchi za Ghana na Nigeria.
Mwaka 2002, Mali ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo na mwaka 2004, ikawa zamu ya Tunisia.
Mwaka 2006, Misri ikawa mwenyeji kabla ya kuipisha Ghana kuandaa mwaka 2008, huku Misri ilifanikiwa kutwaa kombe kwa mara ya pili mfululizo na kuweka rekodi ya kutwa mara sita tangu mwaka 1957.
Kirekodi, Misri ndiyo kinara kwa kutwaa mara hizo sita, ikifuatiwa na nchi za Cameroon na Ghana zilizotwaa mara nne kila moja.
Aidha, Nigeria na DRC, zenyewe zina rekodi ya kutwaa mara mbili kila mmoja na kufuatiwa na Afrika Kusini, Tunisia, Ethiopia, Ivory Coast, Algeria, Congo Brazaville na Morocco zote zikiwa zimetwaa kombe hilo mara moja.
Hivyo, lengo la hii makala ni kuangalia faida kwa nchi mwenyeji wa michuano hii, ingawa suala hilo ni gharama kubwa.
Aidha, ni vigumu kupata fursa ya uenyeji, lakini cha kushangaza ni kuwa baadhi ya nchi zimeweza kuandaa zaidi ya mara mbili au tatu.
Mfano mzuri ni Misri, ambayo inaonekana kuandaa mara nyingi zaidi. Suala la kujiuliza hapa ni kwanini Tanzania ishindwe kuandaa hata mara moja?
Pili, kwa nini waandae mara nyingi hivyo kama michezo hii inakwenda na hasara katika uchumi au madhara yoyote?
Tatu, kwa nini Misri wameandaa mara nyingi? Haya ni maswali ya msingi na ndiyo yaliyonifanya niangalie kiundani faida na hasara za kuandaa mashindano haya, pia ndipo nilipoona umuhimu wa kuandika makala hii.
Uchumi wa Tanzania ni mdogo, lakini hakuna tofauti kati ya Tanzania na nchi kama Mali na Burkina Faso, kwani nchi hizo zimefanikiwa kupata nafasi ya kuandaa mashindano hayo.
Swali la kujiuliza ni kuwa mashindano yameanza tangu mwaka 1957 na kwa nini Tanzania hatujawahi kuandaa mashindano hayo?
Suala la kwanini hatujashiriki au kuwahi kuandaa ni nje ya makala hii na ni suala la viongozi wa michezo na siasa.
Katika makala hii, nitaangalia faida na hasara za kuandaa mashindano haya kwa nchi kama Tanzania.
Kuna kila sababu na ushahidi wa kutosha kuwa nchi inapoandaa mashindano makubwa kama haya yanasaidia kuongeza idadi ya watu wanaoshiriki katika michezo.
Kuna kila sababu ya kwamba nchi inapoandaa kombe kama hilo jamii au watu wanaoishi ndani ya nchi uhamasika na kuwa na msisimko wa kushiriki katika michezo, hii ni kuanzia watoto, vijana hadi wazee.
Hivyo, kuongeza idadi ya watu wanaoshiriki katika michezo ndani ya nchi na kusababisha taifa kuwa na vijana au wazee wenye afya na kupunguza matumizi ya pesa za serikali katika kutibu baadhi ya wagonjwa.
Mfano mzuri, ni wazee wetu wengi wanaugua ugonjwa wa kisukari na ukiangalia zaidi tatizo ni kutokuwa na mazoezi ya kutosha au kutokuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi kabisa.
Faida nyingine za kuandaa mashindano kama haya ni kama ifuatavyo: Kwanza ni viwanja vya michezo na maeneo ya kuajiandaa, nikiwa na maana ya gym.
Nchi inapoandaa mashindano makubwa kama haya husababisha viwanja vya michezo kuangaliwa upya na kuwa na sifa zinazokubalika kimataifa.
Mfano mzuri ni Afrika Kusini, inaandaaa fainali za Kombe la Dunia, ambazo zimesababisha viwanja vya michezo kuangaliwa upya na kujenga vingine, ili kukidhi mahitaji ya maandalizi ya kombe hilo.
Hivyo, nchi kama Tanzania tukiandaa mashindano ya Kombe la Afrika, hii itasababisha viwanja vyetu kuangaliwa upya au kujengwa.
Aidha, njia za usafiri kuimalika, nchi inapoandaa mashindano ya kombe kama hilo hakuna budi kuhakikisha njia za usafiri zinaimalika ili kurahisisha usafiri ndani ya nchi, hasa maeneo mashindano yanapofanyika.
Lakini, mara nyingi baada ya mashindano hayo kumalizika, watakaotumia viwanja hivyo na njia hizo za usafiri ni Watanzania.
Hii itasaidia kuwapatia Watanzania viwanja vizuri na vyenye kukubalika kimataifa kwa ajili ya kuandaa wanamichezo, na njia nzuri za usafiri wa ndani ya nchi.
Pia uchumi; kuna kila sababu ya uchumi wa nchi kukua, hasa kutokana na mambo kama makampuni makubwa kuja nchini kabla ya kuanza na baada ya mashindano, mfano ni makampuni ya utangazaji.
Aidha, utalii, kwani kuna kila sababu ya kwamba panapokuwa na mkusanyiko wa watu wengi kama hivi na kila nchi ina mashabiki au raia wake, kuna kila sababu watakuja kuangalia na kushabikia nchi zao, hasa zinapocheza. Pia wageni hao watasafiri ndani ya nchi ili kuielewa vizuri nchi inayoandaa michuano hiyo.
Nikiwa na maana kutaka kujua vivutio vya kitalii, na hii itasababisha nchi kujulikana kimataifa, hivyo kujiongezea kipato kutokana na utalii.
Aidha, upande wa pili wa shilingi ni nafasi kwa nchi kama Tanzania kujitangaza na kutangaza vivutio vilivyomo nchini.
Faida nyingine, ni maelfu ya ajira kwa wananchi. Hii ni kuanzia ajira ya kudumu na ya muda, kutokana na mashindano kama haya kuhusisha watu wengi na nchi nyingi.
Kuna kila sababu ya kusababisha ajira kwa wananchi wanaokaa maeneo yaliyo karibu na uwanja.
Pia, ajira itapatikana kutokana na utalii. Ajira itapatikana katika maeneo ya utalii, viwandani na katika ujenzi, bila kusahau nyumba za kulala wageni.
Aidha, ni fursa kwa nchi husika kujitangaza kibiashara kupitia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi husika.
Aidha, biashara itapatikana katika maeneo kama ujenzi, viwandani na nyumba za kulala wageni, kwani kuna kila sababu idadi kubwa ya watu itaongezeka kwa kipindi cha muda mfupi na hawa watu watahitaji kula, kulala na kusafiri. Bila kusahau ulinzi, usalama na usafiri.
Katika fainali hizi zitahitajika nyumba mpya kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu watakaokuja, hivyo ni lazima nchi ijiandae kuwa na hoteli nyingi zenye ubora wa kimataifa.
Hii pia huisaidia nchi, kwani baada ya mashindano nchi mwenyeji kwa mfano Tanzania, hubaki na nyumba hizo kwa matumizi yetu ya ndani, hivyo kuepukana na uhaba wa nyumba.
Kuhusu kambi za maandalizi, kutakuwa na ajira na kipato kwa wananchi na nchi ujumla, kwani nchi nyingi hutumia au hufika katika nchi mashindano yanapofanyika wiki moja kabla ya mashindano.
Hii ni kutokana na kutaka kuyazoea mazingira na kuzoea hari ya hewa.
Elimu na ufundi; mashindano kama haya husaidia kuwaandaa watu kielimu na kiufundi hii ni kuanzia na elimu ya michezo, ufundi wa vitendea kazi na mambo mengine muhimu.
Elimu na ufundi; hii ni kwa ajili ya maisha au siku zijazo, kwani baada ya mashindano kwisha, tutabaki na watu wenye elimu na ufundi wa mambo mengi.
Elimu ya utamaduni; kuandaa mashindano kama haya, kunasaidia kuutangaza utamaduni wa nchi na pia nchi au wananchi kujifunza utamaduni wa nchi nyingine.
Aidha, kuandaa mashindano kama haya kutasaidia maeneo yenye au yaliyokuwa na matatizo, mfano umaskini, ulevi, ujambazi na ajira kubadilika kwa faida ya nchi na wananchi.
Hii mara nyingi ni kwa muda na kuendelea, kwani katika uchunguzi (research) ndogo iliyofanyika East London na vijana wa kihuni na wezi, inaonyesha kuwa matukio ya uhalifu hupungua hasa kipindi cha Ligi Kuu inapoanza.
La muhimu zaidi, ni kuwa kutokana na nchi kuandaa mashindano kama hayo kuna kila sababu kuwa mashindano kama haya yatasaidia watu wengi kushiriki katika michezo na hii itasaidia kuwa na taifa lenye afya.
Kwani viwanja vilivyotumika katika mashindano, vitatumiwa na wananchi.
Aidha, kuandaa mashindano kama haya kungesaidia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufanya kazi kwa karibu na klabu za mchezo huu nchini, pia kufanya kazi kwa karibu na Serikali na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Tukiangalia hasara za kuandaa mashindano kama haya, ni kuwa kuandaa ni gharama kubwa.
Aidha, inasemekana kuwa katika kuandaa kombe kama hilo, muda mwingi unatumika na nguvu nyingi.
Kwa kweli, kuna kila sababu kwa Tanzania kuandaa mashindano kama hayo kwani yatasaidia katika kuhamasisha vijana wengi hasa kuipenda soka, kama tunashindwa kushiriki, basi tuandae, kwani kuandaa nako ni pesa kama tunavyoandaa timu.
Hii itasaidia kupata faida nyingi kama ilivyoongelewa hapo juu, lakini la muhimu ni kuwa tutabaki na viwanja vizuri vya michezo, ambavyo vitawasaidia wanasoka wetu kujiandaa vizuri na kuwa na malengo ya muda mrefu.
Huu ndio mtazamo wangu. pia niitakie timu yetu ya taifa kila la heri katika mashindano yaliyoko mbele yao. Mungu ibariki Tanzania.
0 COMMENTS:
Post a Comment