MCHEZO wa ligi kuu ya soka Tanzania bara kati ya Mbeya City fc na Tanzania Prison uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya umemalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Kwenye mchezo huo uliokuwa wa vuta nikuvute, timu zote zilishambuliana kwa zamu katika vipindi vyote viwili lakini hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Kinnah Phiri kwa kuwatoa Issa Nelson, Joseph Mahundi na Ramadhani Chombo, na nafasi zao kuchukuliwa na Michael Kerenge, Ditram Nchimbi na Salvatory Nkulula hayakuweza kubadili matokeo ya mchezo huo uliozikutanisha timu hizi mbili hasimu.
Mara baada ya mchezo Kocha Phiri pamoja na maneno mengine kadhaa alisema kuwa makosa kadhaa kwenye safu ya ushambuliaji yaliinyima City ushindi kwenye mchezo huo.
“Timu imecheza vyema,tutafanyia kazi makosa kadhaa yaliyojitokeza leo kwenye safu yetu ya ushambuliaji, soka iko hivyo, ni jambo jema tumepata pointi moja tunaanza maandalizi ya mchezo ujao tutakaocheza ugenini huko Mlandizi”, alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment