Jul 17, 2010

Posted by Dismas Ten in | Saturday, July 17, 2010 No comments

Inaweza ikawa kama simulizi lakini ukweli ndiyo huo kwamba juzi kati kondakta mmoja mkazi wa Mabatini jijini Mwanza ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alijikuta anapoteza uhai wake baada ya kutokea purukushani ndani ya daladala inayofanya safari yake kati ya Airport na Mwanza mjini.

Sakata lilianza hivi, konda alipakia abiria kutoka Airport kwenda Mwanza mjini, gari lake aina ya Haice lilijaza na kuanza safari, ndipo alipoanza kazi yake kama kawa ya kudai kilichochake.

Nauli kutoka Airport kwenda mjini ni 250/= na katika pita pita yake akajikuta ameishiwa hamsini mfukoni. Kuna abiria mmoja alitaka kushukia njiani hivyo akatoa shingili 500/= ili arejeshewe 250/=. Badala ya kurudishiwa 250/= alipewa 200 kitendo ambacho kilionekana kumkera abiria huyo na kuanza kumtolea konda lugha chafu.

Konda alijibu kwa upole kuwa: “Kaka naomba unisamehe, nimeishiwa chenchi, naomba hiyo hamsini uisamehe siku nyingine ukipanda gari hili utalipa nusu nauli. Mara nyingi nyingi abiri mkisema mmepungukiwa na 50/= huwa tunawaelewa, iweje konda akidai kuishiwa huonekana mkorofi?”

Kauli hiyo ilionekana kama kumchanganya abiria huyo ambaye alionekana kukerwa na maneno hayo ya konda huku yeye akisisitiza kuwa, lazima 50/= yake apewe lasivyo patachimbika. Wakati huo gari lilikuwa katika mwendo kasi huku mzozo huo ukiendelea.

Wakati wote huo konda alijua kama matani kwamba anachokiongea abiria huyo ni jaziba tu atakapofika anapotaka kushuka ataenda zake lakini hali haikuwa hivyo kwani abiria huyo alilazimika kumkunja shati kondakta huyo kwa lengo la kumshinikiza atoe 50/= hiyo.

Purukushani zilionekana kuongeza na abiria huyo kuanza kumsukuma kondakta huyo, mara mlango wa gari hiyo ukachomoka na kujikuta akonda aliyekuwa ameuegemea akipitiwa na taili ya nyuma na kusababisha kifo chake pale pale.

Baada ya gari kusimama na abiria kushuka kwenda kumwangalia kondakita huyo, jamaa aliyesababisha ajali hiyo alitimua mbio na kutokomea kusikojulikana huku wasamalia wema nao wakionekana kutokwa macho kwa kushindwa kuamini walichokiona na kumfanya kila mmoja atokwe na chozi kutokana na kichwa cha konda kutoa mlio kama wayai linapokuwa linachomwa kwenye moto mkali.

Dereva kwa kushirikiana na abiria waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitali ya Bugando kwa ajili ya kuhifadhiwa. Kitendo hicho kilionekana kuwakera abiria wengi huku wengine wakisema kuwa, iweje konda anaposema amepungukiwa 50/= hakubaliki lakini abiria kusema amepungukiwa na konda ionekane ni sahihi.

0 COMMENTS:

TAFUTA HAPA

UNGANA NASI

Delicious Digg Facebook Favorites More Stumbleupon Twitter